Uturuki yatangaza kufikiwa 'suluhu ya kihistoria' kati ya Ethiopia na Somalia
(last modified Thu, 12 Dec 2024 10:33:14 GMT )
Dec 12, 2024 10:33 UTC
  • Uturuki yatangaza kufikiwa 'suluhu ya kihistoria' kati ya Ethiopia na Somalia

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amempongeza Rais wa Somalia na Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa kufikia "suluhu ya kihistoria na kujitolea kwa hali ya juu" katika mazungumzo ya amani baina ya nchi hizo mbili yaliyofanyika mjini Ankara, lengo likiwa ni kumaliza mgogoro wa eneo lililojitenga la Somaliland.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Ankara leo Alkhamisi, Erdogan amemshukuru Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed na kutangaza kuwa pande zote mbili zimekubaliana katika tangazo la pamoja kutatua mgogoro uliopo.

"Tumechukua hatua ya kwanza kuelekea mwanzo mpya uliojikita katika amani na mashirikiano kati ya Somalia na Ethiopia," amesema Erdogan na kuongeza kuwa, tegemeo kubwa la Ankara ni kuleta amani na utulivu, "katika eneo hilo muhimu" la Afrika kati ya Somalia na Ethiopia.

Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa nchi yake inaamini, makubaliano kati ya Somalia na Ethiopia yataweka msingi madhubuti wa mashirikiano na maendeleo yaliyojikita katika misingi ya kuheshimiana.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amepongeza jitihada za Uturuki katika kutatua migogoro ya kikanda na kisiasa kati ya Somalia na Ethiopia, na kuongeza kuwa nchi yake daima imekuwa ikitaka kuwa "rafiki wa kweli na Ethiopia."

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, naye pia amepongeza jitihada za Uturuki na kuyaita makubaliano yaliyofikiwa Ankara kama "mazungumzo ya kifamilia" ambayo yameleta ushindi kwa nchi yake na nchi jirani ya Somalia.

Kwa mujibu wa Tangazo la Ankara, pande zote mbili zimeamua kuanzisha majadiliano ya kiufundi kwa upatanishi wa Uturuki ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari, 2025 na kuyakamilisha katika kipindi cha miezi minne.../