Mazungumzo baina ya Kagame na Tshisekedi huko Angola, yamefutwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120178-mazungumzo_baina_ya_kagame_na_tshisekedi_huko_angola_yamefutwa
Mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo Jumapili kati ya marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC nchini Angola, kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC, yamefutwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Dec 15, 2024 07:25 UTC
  • Kagame na Tshisekedi wanakutana Angola
    Kagame na Tshisekedi wanakutana Angola

Mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika leo Jumapili kati ya marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC nchini Angola, kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa mashariki mwa DRC, yamefutwa.

Maafisa mbalimbali wamesema kuwa, kulikuwa na matarajio makubwa kwamba, Marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wangelikutana leo Jumapili kwa mwaliko wa Rais wa Angola lakini mazungumzo hayo yamefutwa. Mkuu wa ofisi ya Rais wa Angola amewaambia waandishi wa habari kwamba: Kinyume na matarajio yetu,  mkutano hautofanyika leo.

Kwa upande wake ofisi ya rais wa DRC imesema kuwa, mazungumzo hayo hayakufanyika kutokana na masharti yaliyowekwa na Rwanda ya kuitaka Kinshasa ifanye mazungumzo na waasi wa M23 suala ambalo kwa hivi sasa ni mstari mwekundu kwa DRC ambayo inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao. 

Awali, Rwanda ilikuwa imethibitisha kwamba Rais Paul Kagame atashiriki katika mkutano huo akiambatana na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Olivier Nduhungirehe.

Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pia ilikuwa imethibitisha kwambaRais  Felix Tshisekedi atashiriki katika mazungumzo hayo, licha ya awali kukataa kufanya mazungumzo na Rwanda na kutoa mwito wa kuwekwa vikwazo vya kimataifa dhidi ya jirani yake huyo.

"Nchi yetu inaendelea kukabiliwa na uasi, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa jeshi la Rwanda na magaidi wa M23," alisema Tshisekedi wakati akihutubua Bunge la nchi yake Jumatano iliyopita, akiwaita wanamgambo hao na nchi ya Rwanda kuwa "maadui wa Congo DR."

Rais wa Angola, Joao Lourenco, aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi, ameeleza matumaini kwamba Rwanda na DRC zinaweza kufikia makubaliano ya amani.