Takriban watu tisa wameuawa katika shambulizi la droni Darfur, Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120196-takriban_watu_tisa_wameuawa_katika_shambulizi_la_droni_darfur_sudan
Takriban watu tisa wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa kufuatia shambulizi la droni (ndege zisizo na rubani) katika hospitali moja katika mji wa El-Fasher katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.
(last modified 2024-12-15T23:10:30+00:00 )
Dec 15, 2024 23:10 UTC
  • Takriban watu tisa wameuawa katika shambulizi la droni Darfur, Sudan

Takriban watu tisa wameuawa na wengine 20 kujeruhiwa kufuatia shambulizi la droni (ndege zisizo na rubani) katika hospitali moja katika mji wa El-Fasher katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Jana Wizara ya Afya ya Serikali ya Shirikisho la Sudan ililalamika kwamba, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) ndivyo vilivyohusika na shambulio hilo la siku ya Ijumaa.

Maafisa wa wizara hiyo wamesema kwamba kundi hilo lilirusha maguruneti manne na kupiga kituo kikuu cha afya cha mji huo.

Nayo kamati ya upinzani huko el-Fasher inayohusika na juhudi za kutoa misaada imesema kwamba, shambulio hilo lililenga hospitali ya Saudi na kuilazimisha kusimamisha huduma za matibabu. Imesema: Hiyo ndiyo hospitali ya mwisho iliyokuwa inafanya kazi mjini humo.

Jeshi la Sudan na kukndi la RSF wamekuwa wakipigana huko el-Fasher tangu Mei 10 mwaka huu. Mji huo ni kitovu cha juhudi za kibinadamu za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada ya kimataifa huko Darfur.

Shambulio hilo la Ijumaa ni la karibuni zaidi katika wimbi la mashambulio mabaya yaliyotokea kwenye eneo hilo wiki hii.

Jumatatu ya wiki iliyopita, zaidi ya watu 100 - ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto - waliuawa katika shambulio la anga kwenye soko moja la wazi la mji wa Kabkabiya, kaskazini mwa Darfur. Mji huo uko umbali wa takriban kilomita 180 kutoka El-Fasher.