Takriban watu 15 wameuawa katika shambulio la wanamgambo magharibi mwa Sudan
Shirika la habari la serikali ya Sudan SUNA limeripoti kuwa, shambulio la ndege zisizo na rubani lililofanywa na wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) limeua zaidi ya watu 15 katika soko moja huko El Fasher, magharibi mwa Sudan.
Taarifa ya shirika hilo la habari imesema kuwa, shambulizi hilo lilipiga soko la kitongoji cha Awlad Al-Reef saa nne na nusu usiku kwa saa za eneo hilo. Taarifa hiyo imewanukuu watu walioshuhudia wakisema kuwa, watu wengine wengi wamejeruhiwa na kuwahishwa hospitalini.
Mbali na hayo, Jeshi la Sudan (SAF) limetangaza kuwa, limezima jaribio la wanamgambo wa RSF la kuingia katika mji wa El Fasher kutokea maeneo ya kusini Sudan, juzi Jumamosi.
Jeshi hilo la Sudan SAF limedai kuwa limewasababishia hasara kubwa wanamgambo wa FSR na kuua wapiganaji 20 na kuharibu magari saba ya kivita na kuyateka nyara mengine. Hata hivyo kundi la RSF halikuweza kupatikana haraka kuwezo kutoa maoni yake kuhusu tukio lolote.
Mapigano kati ya majenerali wa kijeshi wanaoongozwa makundi mawili ya SAF na RSF yamepamba moto kwenye mji wa El Fasher tangu Mei 10.
Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali hao wa kijeshi vilianza tarehe 15 Aprili 2023 na vimeshaua zaidi ya watu 28,700 na kuwalazimisha zaidi ya milioni 14 wengine kuyahama makazi yao. Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za mashirika ya kimataifa.