Rais wa Angola alaani uvamizi wa madola ya kigeni nchini Syria
Rais Joao Lourenco wa Angola amelaani uvamizi wa madola ya kigeni nchini Syria na ameelezea masikitiko yake kutokana na kuvamiwa na kukaliwa kwa mabaru ardhi za nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika sehemu moja ya matamshi yake, Rais Lourenco amesema: "Kukosekana uhakika wa maisha nchini Syria pamoja na mabadiliko ya hivi karibuni baada ya kupinduliwa serikali iliyokuwepo madarakani, ni mambo ambayo yanachochea tamaa hatari ya baadhi ya madola ya kigeni ya kutaka kumiliki sehemu za ardhi ya Syria."
Ameyasema hayo kwenye hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa dharura wa chama cha PMLA mjini Luanda, yeye akiwa ni mwenyekiti taifa wa chama hicho tawala.
Vilevile amesema kuwa, vita, ugaidi na mabadiliko ya tawala kinyume cha Katiba katika nchi za Afrika, Asia Magharibi hasa Syria na matukio ya barani Ulaya ni mambo ambayo yanazidi kutishia amani na usalama duniani.
Aidha ametoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya umati yanayofanywa na Israel dhidi ya wananchi wa Palestina huko Ghaza na ametaka kufanyike mazungumzo ya kutatuliwa haraka mgogoro wa Ghaza na wa Palestina kiujumla.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake amesema: "Hakuna mtu anayeweza kuwanyima Wapalestina haki yao ya kimsingi kabisa, nayo ni ya kuishi kwa amani katika ardhi yao wenyewe. Hivyo jaribio lolote la kuwafukuza raia hao katika nchi yao na kuwahamishia nchi jirani lazima lizimwe mara moja na kikamilifu."