Afisa wa Umoja wa Mataifa yuko CAR kuimarisha mchakato wa kurejesha amani
-
Jean-Pierre Lacroix
Katika siku ya pili ya ziara yake nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Jean-Pierre Lacroix, mkuu wa mpango wa amani wa Umoja wa Mataifa, amekutana na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Felix Moloua ambapo viongozi hao wawili wamejadili hali ya sasa ya nchi hiyo na hatua muhimu zinazohitajika kwa ajili ya kuberesha mwenendo wa kurejesha amani.
Hali ya kibinadamu na usalama nchini CAR imezorota tangu Machi, huku kukiwa na ongezeko la mapigano kati ya makundi yenye silaha. Licha ya changamoto hizo, mafanikio makubwa yamepatikana katika kurejesha utulivu nchini humo.
Katika mazungumzo hayo, Lacroix amegusia maeneo kadhaa yenye mabadiliko chanya ikiwa ni pamoja na kurejeshwa mamlaka ya serikali katika maeneo yenye migogoro na juhudi za kurejesha utulivu katika mikoa mbalimbali ya nchi hiyo.
Afisa huyo wa UN pia ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika kuwapokonya silaha wanachama wa makundi ya waasi, na ukweli kwamba baadhi ya makundi hayo yamejiondoa katika migogoro ya silaha na kurejea tena katika maisha ya kiraia.
Hata hivyo, mada kuu zaidi ya mazungumzo hayo ni mchakato wa uchaguzi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati uliopangwa kufanyika mwaka ujao. Lacroix amesisitiza umuhimu wa kujiandaa kwa ajili ya makabidhiano salama ya madaraka na mchakato wa upigaji kura wa haki na uadilifu.
Mazungumzo hayo pia yamejikita katika njia za kuwalinda raia na kuimarisha uwajibikaji wa nchi hiyo kwa sheria za kimataifa za kibinadamu.