Rais wa Algeria asisitiza nia yake ya kweli ya kupambana na ufisadi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120816-rais_wa_algeria_asisitiza_nia_yake_ya_kweli_ya_kupambana_na_ufisadi
Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ametilia mkazo dhamira ya serikali yake ya kupambana na ufisadi na ubadhirifu, na kuahidi kuanzisha mazungumzo kitaifa ili kutatua changamoto za ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2024-12-30T23:21:31+00:00 )
Dec 30, 2024 23:21 UTC
  • Rais wa Algeria asisitiza nia yake ya kweli ya kupambana na ufisadi

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ametilia mkazo dhamira ya serikali yake ya kupambana na ufisadi na ubadhirifu, na kuahidi kuanzisha mazungumzo kitaifa ili kutatua changamoto za ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika.

Tebboune amesema  hayo wakati alipokuwa anahutubia mabaraza yote mawili ya bunge mjini Algiers na kusisitiza kwa kusema: "Tumefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kuleta uadilifu ili kurejesha imani ya wananchi kwa serikali. Tumehakikisha kuna usawa pia katika mgawanyo wa fedha na rasiliamali za taifa baina ya watu wote na tunapambana na ufisadi bila ya kuchoka."

Rais wa Algeria ametangaza pia mipango ya serikali yake ya kuwa na mazungumzo ya kisiasa kitaifa kwa lengo la kushughulikia changamoto za ndani za Algeria na kuimarisha haki za kimsingi kwa kila mwananchi bila ya ubaguzi wowote.

Rais Tebboune aidha amesema: "Mazungumzo haya yatakuwa ya kina, ya kujumuisha watu wa kada na matabaka yote na yatakuwa mbali na maneno ya kujirudiarudia."

Amesema, serikali yake itahakikisha kwamba mazungumzo hayo yanafanyika kwa njia sahihi iliyopangwa na ya uwazi, kwa lengo la kukuza umoja na mshikamano na kuimarisha maelewano ya ndani la Algeria.