Pezeshkian amwambia Macron: Iran yataka diplomasia huku ikisisitiza kulinda haki za taifa
-
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian (kulia) na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron,
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, amemwambia mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, kuwa Tehran iko tayari kuendelea kwa dhati kupitia njia za kidiplomasia ili kukomesha vita, huku ikisisitiza umuhimu wa kulindwa kwa haki za taifa la Iran.
Rais Pezeshkian amesisitiza tena kuwa Iran haiiamini Marekani katika mazungumzo hayo, akisema hali hiyo imetokana na Marekani kuanzisha vita mara mbili wakati wa mazungumzo yaliyopita.
Katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika Jumatano, marais hao wawili walijadili hali ya kimkakati katika eneo hilo, hususan suala la Mlango wa Hormuz, pamoja na hatua za makubaliano ya kusitisha mapigano kwa muda na mwendelezo wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Pezeshkian alisema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, iko tayari kusimamia kwa umakini njia za diplomasia ili kumaliza vita, huku tukisisitiza utekelezaji wa haki za taifa la Iran.”
Katika mazungumzo hayo, marais wa Iran na Ufaransa pia walibadilishana mitazamo kuhusu hali ya Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya baharini ambayo Iran imeiweka chini ya uangalizi mkali tangu kuanza kwa vita.
Mazungumzo hayo ya simu pia yaliangazia makubaliano ya awali ya kusitisha vita na juhudi za upatanishi zinazoongozwa na Pakistan.
Tangu mapema Aprili, kumekuwepo sitisho tete la vita, lakini mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Tehran na Washington yamesimama, huku Iran ikiituhumu Marekani kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita kupitia mzingiro wa kijeshi baharini na vitisho vya kijeshi.
Ufaransa imekuwa miongoni mwa nchi za Ulaya zilizoendelea kudumisha njia za mawasiliano ya kidiplomasia na Tehran katika kipindi chote cha mgogoro huo.
Mazungumzo kati ya Iran na Marekani bado hayajazaa matunda, huku Iran ikitaka kuondolewa kwa mzingiro wa baharini, kusitishwa kikamilifu kwa vita, pamoja na fidia kwa uharibifu uliosababishwa na hujuma za Marekani na Israel.