China yalaani vita dhidi ya Iran, yataka usitishaji kamili wa mapigano
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi,
China imemkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, kwa mazungumzo mjini Beijing, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, akivitaja vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran kuwa “visivyo halali” na kutoa wito wa kusitishwa kabisa kwa mapigano.
Wang Yi, mwanadiplomasia mkuu wa China, alikutana na Araghchi mjini Beijing Jumatano na kusisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa usitishaji kamili wa mapigano katika eneo la Asia Magharibi.
Wang amesema: “Tunaamini kwamba usitishaji wa mapigano wa kina unahitajika kwa dharura, kwamba kurejea kwa mapigano hakukubaliki, na ni muhimu sana kuendelea na dhamira ya mazungumzo na majadiliano.”
Pia amekosoa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akisema kuwa “eneo hili linapitia kipindi muhimu cha mabadiliko, na mikutano ya moja kwa moja kati ya pande husika ni jambo la lazima.”
Araghchi ameishukuru China kwa msimamo wake thabiti, hasa kwa kulaani Marekani na Israel, akieleza kuwa Beijing ni rafiki wa kweli wa Tehran. Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Iran na China utaimarika zaidi katika mazingira ya sasa.
Araghchi amesema vita dhidi ya Iran ni “uchokozi wa wazi na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.”
Akirejea njia ya kidiplomasia, amesisitiza kuwa Iran itatumia uwezo wake wote katika mazungumzo ili kulinda haki na maslahi yake halali, akibainisha kuwa Tehran haitaridhika na chochote kisicho “makubaliano ya haki na ya kina.”
Waziri huyo wa Iran aliwasili Beijing Jumatano asubuhi akiongoza ujumbe wa kidiplomasia.
Ziara hiyo imefanyika baada ya angalau mazungumzo matatu ya simu kati ya Wang na Araghchi tangu kuanza kwa vita dhidi ya Iran tarehe 28 Februari. Mazungumzo yao ya mwisho yalifanyika Aprili 15, ambapo Araghchi alisifu msimamo wa kuwajibika wa China na Russia katika kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoungwa mkono na Marekani dhidi ya Iran, akisema hatua hiyo ilisaidia kuzuia kuongezeka kwa mvutano.
Wang pia amesifu ustahimilivu wa wananchi wa Iran wakati wa vita vya karibuni na kusisitiza tena utayari wa Beijing kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza vita.
Wachambuzi wanasema ziara hiyo, inayofanyika siku chache kabla ya safari ya Rais wa Marekani, Donald Trump, mjini Beijing, imepangwa kimkakati.
Mwezi uliopita, China iliungana na Russia kutumia kura ya turufu dhidi ya azimio lililoungwa mkono na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililolenga Iran.