Iran imewasilisha nyaraka kuhusu jinai za kivita za Marekani na Israel
-
Picha za baadhi ya watoto waliouawa katika hujuma ya kigaidi iliyotekelezwa na Marekani tarehe 28 Februari 2026 katika shule ya Minab, Iran
Mkuu wa Shirika la Hilali Nyekundu la Iran amesema wamewasilisha nyaraka 35 zinazoonyesha wazi jinai za kivita zilizofanywa na Marekani na Israel wakati wa mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Iran, katika taasisi mbalimbali za kimataifa.
Akizungumza katika mkutano wa habari mjini Tehran, Pirhossein Kolivand amebainisha kuwa Hilali Nyekundu imeziarifu taasisi za kimataifa kuhusu ukubwa na aina ya jinai za kivita za Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Amesema: “Mojawapo ya mafanikio yetu katika uwanja huu ni kwamba tulimwomba Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu akubali hati zilizowasilishwa na Hilali Nyekundu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama vielelezo rasmi.”
Ameongeza kuwa hadi sasa shirika hilo “limeandikisha nyaraka 35 za ukiukaji” wa sheria za kimataifa za kibinadamu uliofanywa na Marekani na Israel katika vita dhidi ya Iran.
Kolivand amesisitiza kuwa: “Ukizitazama mahojiano ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, utaona kwamba baada ya barua ya ishirini, wanaashiria kuwa hawaitambui Israel kama nchi.”
Amesema pia kuwa wawakilishi wa taasisi kadhaa za kimataifa wamefika Iran, akiongeza kuwa mwakilishi mmoja wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba yeye “atakuwa sauti ya wananchi wa Iran.”
Aidha, ametangaza kuwa ujumbe kutoka Hilali Nyekundu ya Iran utasafiri kwenda Geneva katikati ya mwezi Juni ili kuyafahamisha mataifa mengine kuhusu jinai za wazi na zisizofichika za utawala wa Kizayuni na Marekani.
Afisa huyo amesema kuwa jitihada za Iran katika kufuatilia hatua za kisheria dhidi ya wavamizi zinafuata maelekezo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Shahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ambaye alifikia hadhi ya shahidi siku ya kwanza ya mashambulizi ya Marekani na Israel, aliposisitiza kuwa mamlaka za nchi lazima zitafute haki za taifa kupitia njia za kisheria.
Kolivand amesema: “Kiongozi wetu aliyeuawa kishahidi alitukumbusha kwamba hata kama mambo mengine hayafanyi kazi, ‘lazima mfanye kazi yenu ya kisheria.’ Sasa, tutakuwa na mkutano wa mtandaoni wiki ijayo na wataalamu kadhaa wa sheria za kimataifa za kibinadamu walioko nchi mbalimbali, ili kuwafahamisha upeo wa jinai hizi na kutusaidia katika kudai haki.”
Ameongeza kuwa: “Kwa maneno mengine, tunaunda muafaka wa kimataifa.”
Tawala dhalimu za Marekani na Israel zilianzisha duru mpya ya vita vya kigaidi dhidi ya Iran tarehe 28 Februari, takriban miezi minane baada ya mashambulizi mengine ya kichokozi dhidi ya nchi hii.