ODM yaionya serikali ya Kenya kuhusu utekaji, yatishia kuitisha uasi wa kiraia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120830-odm_yaionya_serikali_ya_kenya_kuhusu_utekaji_yatishia_kuitisha_uasi_wa_kiraia
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kimetoa onyo kali, kikitishia kuongoza uasi wa kiraia dhidi ya utawala wa Rais William Ruto wa Kenya kutokana na kile kinachosema ni kuibuka siasa za kidikteta na dhuluma.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 31, 2024 04:12 UTC
  • Prof Anyang’ Nyong’o
    Prof Anyang’ Nyong’o

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinachoongozwa na Raila Odinga kimetoa onyo kali, kikitishia kuongoza uasi wa kiraia dhidi ya utawala wa Rais William Ruto wa Kenya kutokana na kile kinachosema ni kuibuka siasa za kidikteta na dhuluma.

Kwa mujibu wa mtandao wa Taifa Leo, kiongozi wa muda wa chama cha ODM, Prof Anyang’ Nyong’o, ambaye ni Gavana wa Kisumu amekosoa visa vya utekaji nyara vinavyoendelea kote nchini Kenya akisema watapinga majaribio ya serikali ya kuwakandamiza Wakenya.

“Tuko tayari kuongoza uasi dhidi ya siasa za kidikteta na dhuluma ambazo zinajaribu kulazimisha utawala dhalimu na usio wa kidemokrasia kwa watu kupitia mambo kama vile utekaji nyara na vitisho vya kisiasa,” amesema Prof Nyong’o.

Ameongeza kuwa: “Tunaitaka sana serikali ikomeshe utekaji nyara huu wa woga wa wale wanaokosoa sera zisizo za kidemokrasia.”

Awali kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga alikuwa ameonya kwamba Wakenya hawawezi kuvumilia utekaji nyara akiutaja kuwa ni ujambazi.

Jana Jumatatu, polisi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, wamefyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wanaopinga kile wanachosema ni wimbi la utekaji nyara wa wakosoaji wa serikali bila sababu.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema, makumi ya Wakenya wametekwa nyara katika miezi ya hivi karibuni na yanahusisha vitendo hivyo vya utekaji na polisi na idara za kijasusi za Kenya.

Mamlaka za Kenya zimepinga madai hayo.