Afrika Mashariki: Mjumbe wa IGAD kuzuru Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120838-afrika_mashariki_mjumbe_wa_igad_kuzuru_sudan
Mjumbe wa Jumuiya ya nchi za IGAD Lawrence Korbandy anatarajiwa kuzuru nchini Sudan mwezi Januari kujaribu kusuluhisha mzozo unaoendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa wakipigana tangu mwezi Aprili mwaka 2023.
(last modified 2024-12-31T08:08:44+00:00 )
Dec 31, 2024 08:08 UTC
  • Afrika Mashariki: Mjumbe wa IGAD kuzuru Sudan

Mjumbe wa Jumuiya ya nchi za IGAD Lawrence Korbandy anatarajiwa kuzuru nchini Sudan mwezi Januari kujaribu kusuluhisha mzozo unaoendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa wakipigana tangu mwezi Aprili mwaka 2023.

Jitihada hizi za usuluhishi zinatarajiwa kufanyika wakati Sudan ina uhusiano baridi na Jumuiya ya IGAD ambayo iliisimamisha uanachama kutokana na vita vinavyoendelea.

Mjumbe huyo atarejea Sudan, baada ya jitihada za hapo awali zilizoongozwa na IGAD, Marekani na Saudi Arabia kujaribu kuwaleta Majenerali Mohamed Hamdan Daglo anayeongoza RSF na mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan kwenye meza ya mazungumzo, kugonga mwamba.

Mwezi Januari, IGAD ilialika pande mbili zinazozana kwenye kikao cha pamoja jijini Kampala, lakini mkutano huo haukufanyika baada ya uongozi wa kijeshi kudai kuwa Jumuiya hiyo ilikuwa inaingilia mambo yake ya ndani.

Korbandy amesema anatumai kuwa ziara yake itasaidia kumaliza vita hivyo ambavyo vimesabisha vifo vya maelfu ya watu na kuwaacha wengine zaidi ya Milioni 12 kuyakimbia makaazi yao.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi nchini Sudan vimesababisha zaidi ya watu 80,000 kukimbilia Sudan Kusini katika muda wa chini ya wiki tatu. Wengi wao wamekwama mpakani.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ambalo limeongeza kuwa, wengi wa wakimbizi hao ni wanawake na watoto wadogo.