Waasi wa ADF wazidisha mashambulio mashariki mwa DRC
Juhudi zote za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo za kukabiliana na kusonga mbele waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo zinaendelea huku mashambulio ya waasi wenye mfungamano na kundi la Allied Defence Forces (ADF), yanaendelea katika eneo la Béni, inayopakana na Uganda.
Kushadidi mashambulio ya waasi hao kunaelezwa kuwa, huenda kukakwamisha na kuzorotesha operesheni zilizokuwa zikishika kasi za jeshi dhidi ya waasi wa M23.
Janvier Kasayiryo, rais wa vijana wa eneo la Béni, “Kuanzia Novemba 17 hadi Desemba 14, tulirekodi mashambulizi 11 ya ADF, ambayo yalisababisha vifo vya watu 25.
Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) wameua watu wasiopungua 21 katika mashambulio kadhaa waliyofanya katika wiki ya Krismasi kwenye eneo lililokumbwa na mgogoro wa vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Oktoba mwaka huu Rais Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo alithibitisha uamuzi wa nchi yake wa kuendeleza ushirikiano wa kijeshi kati yake na Jeshi la Uganda UPDF katika vita dhidi ya waasi wa ADF huko Kivu Kaskazini na Ituri nchini DRC.
Kundi la ADF ni maarufu kwa vitendo vyake vya uhalifu na jinai katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri ambayo yamezingirwa na jeshi la Kongo tangu mwezi Mei 2021, huku maafisa kijeshi na polisi wakichukua nafasi za utawala kutoka kwa raia.