Askari 13 DRC wahukumiwa kifo katika jitihada za kuimarisha nidhamu jeshini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i120898-askari_13_drc_wahukumiwa_kifo_katika_jitihada_za_kuimarisha_nidhamu_jeshini
Mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetoa hukumu ya kifo kwa wanajeshi 13 kwa makosa ya mauaji, uporaji, na woga katika hatua ambayo inalenga kuboresha nidhamu ya jeshi. Hukumu hizi zimetolewa Jumanne katika mji wa Lubero, Kivu Kaskazini, ambako vikosi vya Congo vimekuwa vikikabiliana na uasi hasa ule  wa kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
(last modified 2025-01-01T23:11:22+00:00 )
Jan 01, 2025 23:11 UTC
  • Askari 13 DRC wahukumiwa kifo katika jitihada za kuimarisha nidhamu jeshini

Mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetoa hukumu ya kifo kwa wanajeshi 13 kwa makosa ya mauaji, uporaji, na woga katika hatua ambayo inalenga kuboresha nidhamu ya jeshi. Hukumu hizi zimetolewa Jumanne katika mji wa Lubero, Kivu Kaskazini, ambako vikosi vya Congo vimekuwa vikikabiliana na uasi hasa ule  wa kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Msemaji wa jeshi la eneo hilo, Mak Hazukay, amesema visa vya wanajeshi kuacha nafasi zao vimewasaidia maadui kusonga mbele, hivyo kupelekea kuandaa kesi hii ya kielimu ili kuweka mambo sawa.

 Kwa jumla, wanajeshi 24 walifikishwa mahakamani, ambapo wanne walipata hukumu ya miaka 2-10, sita waliachiliwa huru, na kesi ya mmoja iliahirishwa kwa uchunguzi zaidi.

Wote waliopatikana na hatia walikana mashtaka na wana siku tano za kukata rufaa dhidi ya hukumu yao.

Hayo yanajiri wakati ambao juhudi za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo za kukabiliana na kusonga mbele waasi wa M23 mashariki mwa nchi hiyo zinaendelea huku mashambulio ya waasi wenye mfungamano na kundi la Allied Defence Forces (ADF), yakiendelea katika eneo la Béni, inayopakana na Uganda.

Kushadidi mashambulio ya waasi hao kunaelezwa kuwa, huenda kukakwamisha na kuzorotesha operesheni zilizokuwa zikishika kasi za jeshi dhidi ya waasi wa M23.

Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) wameua watu wasiopungua 21 katika mashambulio kadhaa waliyofanya katika wiki ya Krismasi kwenye eneo lililokumbwa na mgogoro wa vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.