Wahamiaji 27 wafariki baada ya boti kuzama mashariki mwa pwani ya Tunisia
Wahamiaji 27 wakiwemo wanawake na watoto, wamepoteza maisha wakati boti mbili zilipozama kwenye pwani ya mashariki mwa Tunisia, huku watu 83 waliokolewa.
Zied Sdiri, mkuu wa ulinzi wa kiraia katika mji wa Sfax amesema maafisa wa Tunisia wamesema wahamiaji hao walikuwa njiani kuelekea Ulaya, wakitokea katika nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika.
Msako unaendelea kwani kuna uwezekano wa kuwapata abiria wengine ambao wametoweka. Tunisia ni kituo kikuu cha kuondokea kwa wahamiaji ambao wanataka kufika Ulaya kupitia Italy, ambako wanafika katika kisiwa cha Lampedusa kiasi cha kilometa 150 kutoka Tunisia, mara nyingi hicho ndiyo kituo chao cha kwanza.
Kila mwaka, maelfu ya watu wanajaribu kutumia njia hatari ya kuvuka bahari ya Mediterranean, ambayo inaonekana kujaa boti chakavu, huku kukiwa na hatari zilizochangiwa na hali mbaya ya hewa.
Hapo Desemba 18, takriban wahamiaji 20 kutoka Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara walifariki katika ajali ya boti kwenye mji wa Sfax.