Ethiopia na Somalia zakubaliana kushirikiana katika kudumisha amani
Ethiopia na Somalia zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOOM).
Hii ni kufuatia ziara bi Aisha Mohammad Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia huko Somalia.
Hii ni ziara ya kwanza ya pande mbili kufanywa tangu uhusiano wa nchi mbili hizo jirani kuingia dosari mwaka mmoja uliopita baada ya Ethiopia kutangaza mpango wa kujenga kituo cha jeshi la wanamaji katika eneo lililojitenga na Somalia la Somaliland.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia leo imetangaza kuwa nchi hiyo na Somalia zimekubaliana kufanya kazi pamoja katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM) na kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita liliidhinisha kikosi cha kudumisha amani nchini Somalia kwa jina la AUSSOM kuchukua nafasi ya oparesheni kubwa ya kupambana na ugaidi ya Umoja wa Afrika (AU) kuanzia tarehe Mosi mwezi huu wa Januari.
Wanachama 14 kati ya 15 wa Baraza la Usalama walipiga kura kuunga mkono azimio hilo lakini Marekani ilijizuia kupiga kura.
Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zimetakiwa kuchukua hatua zote zinazohitajika kwa muda wa miezi 12, ikiwa ni pamoja na kuiunga mkono serikali ya Somalia kuyaangamiza makundi ya al-Shabaab na Daesh.