Mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu yaanza nchini Gambia
Mashindano ya kimataifa ya kuhifadhi Qur'ani Tukufu yameanza nchini Gambia kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi 28.
Katika mashindano hayo yaliyoanza jana Jumanne kwa anwani ya kumbukumbu za mwaka wa 22 wa mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1994 nchini humo ambayo yanatambuliwa na serikali ya Banjul kama mapinduzi ya kitaifa. Waandaaji wa mashindano hayo wamewashajiisha Waislamu kusoma na kufahamu mafundisho adhimu ya kitabu hicho cha mbinguni na kwamba kutalii na kufahamu Qur'ani kutasaidia kutatua matatizo ambayo yanawakabili Waislamu hii leo. Katika ufunguzi wa mashindano hayo,
Fatou Lamin Faye, Waziri wa Elimu ya Msingi wa Gambia amesema kuwa, vitendo vya watu wenye kufurutu ada na ugaidi vimesababisha dini ya Uislamu na Waislamu kwa ujumla kutiliwa shaka kiasi kwamba hii leo kila Mwislamu anafuatiliwa kwa kudhaniwa kuwa gaidi. Waziri wa Elimu ya Msingi nchini Gambia ameongeza kuwa, mienendo ya magaidi hao wanaojiita wafuasi wa Uislamu, imewasababishia Waislamu wa kweli changamoto nyingi katika kutetea Uislamu.
Katika mashindano hayo, washiriki kutoka nchi 28 za Afghanistan, Burkina Faso, Cameroon, Chad, Côte d’Ivoire, Jordan, Tunisia, Lebanon, Malaysia, Mali, Mauritania, Niger, Nigeria, Oman, Pakistan, Palestina, Senegal, Somalia, Tunisia, Uturuki, Uganda, Yemen, Benin, Qatar, na Gambia, wanachuana vikali. Aidha majaji kutoka Lebanon, Misri, Uturuki, Senegal, Morocco, Algeria na Gambia wanasimamia mashindano hayo.