Waziri wa Mambo ya Nje wa China kutembelea nchi Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121010-waziri_wa_mambo_ya_nje_wa_china_kutembelea_nchi_afrika
Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi atatembelea nchi kadhaa za Afrika huku Beijing ikiwa mbioni kujiimarisha katika bara hilo pamoja na kuwepo ushindani mkubwa kutoka madola ya Magharibi.
(last modified 2025-01-04T09:57:40+00:00 )
Jan 04, 2025 09:57 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa China kutembelea nchi Afrika

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi atatembelea nchi kadhaa za Afrika huku Beijing ikiwa mbioni kujiimarisha katika bara hilo pamoja na kuwepo ushindani mkubwa kutoka madola ya Magharibi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning amesema., "Mwanachama wa Ofisi ya Kisiasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi atatembelea Namibia, Jamhuri ya Kongo, Chad na Nigeria kuanzia Januari 5 hadi 11 kwa mwaliko."

Mnamo Septemba, Rais wa China Xi Jinping alisema Beijing iko tayari kuimarisha imani ya kimkakati na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na nchi za Afrika.

Pia alibainisha kwamba China iko tayari kushirikiana na nchi za Afrika kwa ajili ya ulimwengu wa kimataifa wenye usawa na mpangilio, utandawazi wa kiuchumi unaojumuisha manufaa kwa wote, pamoja na kulinda haki na usawa wa kimataifa kwa pamoja.

Aida Rais wa China Xi Jinping aliaahidi kuunda nafasi za kazi zaidi ya milioni moja barani Afrika huku akijaribu kuiweka Beijing kama mshirika bora wa maendeleo kwa nchi za Eneo la Kusini mwa Dunia. Akizungumza kwenye Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika alisema Beijing itatoa dola bilioni 51 kwa nchi za Afrika katika ufadhili mpya, ikiwa ni pamoja na mikopo na "aina mbalimbali za misaada", na kuunga mkono miradi 30 ya miundombinu ili kuimarisha mawasiliano katika bara zima.