Watu 8 wauawa na wengine 53 wajeruhiwa katika mashambulizi mapya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121040-watu_8_wauawa_na_wengine_53_wajeruhiwa_katika_mashambulizi_mapya_sudan
Takriban watu wanane wameuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika shambulizi la mizinga lililofanywa na Wanajeshi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika mji mkuu wa Sudan Khartoum na mji wa El Fasher wa Jimbo la Darfur Kaskazini.
(last modified 2025-01-05T07:55:53+00:00 )
Jan 05, 2025 07:55 UTC
  • Watu 8 wauawa na wengine 53 wajeruhiwa katika mashambulizi mapya Sudan

Takriban watu wanane wameuawa na wengine 53 kujeruhiwa katika shambulizi la mizinga lililofanywa na Wanajeshi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika mji mkuu wa Sudan Khartoum na mji wa El Fasher wa Jimbo la Darfur Kaskazini.

Wizara ya Afya ya Mkoa wa Khartoum imetangaza habari hiyo na kuandika: "Wanamgambo wa RSF wameendelea na mashambulizi yao dhidi ya raia katika eneo la Karari la mji wa Omdurman, kaskazini mwa Khartoum na Sharq Alneel (Nile Mashariki) na kuua raia 4 na kujeruhi wengine 43."

Taarifa hiyo pia imesema: "Majeruhi wamehamishiwa kwenye Hospitali za "Al-No" na "Abu Sied" huko Omdurman na katika Hospitali ya "El Ban Jadid" ya eneo la Sharq Alneel."

Jana Jumamosi, Jeshi la Sudan SAF lilitangaza kwamba, raia wanne wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa katika shambulio la makombora na RSF lililofanywa juzi Ijumaa kwenye vitongoji vya makazi ya raia huko El Fasher. Hadi wakati tunaandaa taarifa hii, RSF walikuwa bado hawajatoa maelezo yoyote kuhusu madai hayo. 

Tangu Mei 10, 2024, mapigano makali kati ya SAF na RSF yamekuwa yakiendelea huko El Fasher.

Sudan imekumbwa na mapigano ya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya mwezi Aprili 2023. 

Zaidi ya watu 29,683 wameshauwa na milioni 14 wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan. Hayo ni kwa mujibu wa makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa.