Kiongozi wa upinzani Msumbiji asema atarudi nyumbani kutoka uhamishoni wiki hii
Jan 06, 2025 02:37 UTC
Kiongozi wa upinzani wa Msumbiji ambaye akiwa uhamishoni nje ya nchi, amekuwa akiongoza maandamano ya zaidi ya miezi miwili dhidi ya matokeo ya uchaguzi yaliyozusha utata ametangaza kuwa, atarejea nchini humo wiki hii kabla ya kuapishwa rais mpya.
"Alkhamisi, Januari 9, saa 8:05 juu ya alama, Venancio Mondlane atakuwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mavalane," ameeleza hivyo kiongozi huyo wa upinzani katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa Facebook mubashara jana Jumapili.
Mondlane aliondoka Msumbiji Oktoba 21, akisema anahofia maisha yake alipokuwa akipinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 9 ambayo yalimtangaza kuwa mshindi wa pili akitanguliwa na Daniel Chapo mgombea wa chama tawala cha Frelimo aliyetangazwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho.
Rais mteule Chapo anatarajiwa kuapishwa Januari 15.
Maandamano makubwa ya upinzani yaliyogubikwa na machafuko yalizuka nchini Msumbiji baada ya uamuzi wenye utata uliotolewa na mahakama kuthibitisha ushindi wa mgombea wa chama tawala cha Frelimo, ambacho kimekuweko madarakani tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni wa Kireno mwaka 1975.
Muda mchache tu baada ya tangazo hilo la mahakama, maandamano yalizuka nchini kote Msumbiji, ambapo ofisi za Frelimo, vituo vya polisi, mabenki, na viwanda vimeporwa na kuchomwa moto katika siku chache zilizopita.
Aidha, zaidi ya wafungwa 1,500 walitoroka gereza lenye ulinzi mkali baada ya kuangusha ukuta wake wakati machafuko ya kisiasa yalipokuwa yakiendelea kufuatia uchaguzi wa Oktoba ambao matokeo yake yameibua utata. Makabiliano yaliyotokea wakati wa kutoroka wafungwa hao yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 30 mbali na wengine wengi waliojeruhiwa. Wafungwa wapatao 150 walikamatwa tena baadaye.../