Mkuu wa Jeshi la Uganda: Ninataka kumkata kichwa Bobi Wine
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121090-mkuu_wa_jeshi_la_uganda_ninataka_kumkata_kichwa_bobi_wine
Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni, amesema anataka kumkata kichwa kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo Robert Kyagulanyi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Bobi Wine.
(last modified 2025-01-06T09:44:33+00:00 )
Jan 06, 2025 09:44 UTC
  • Mkuu wa Jeshi la Uganda: Ninataka kumkata kichwa Bobi Wine

Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni, amesema anataka kumkata kichwa kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini humo Robert Kyagulanyi ambaye ni mashuhuri kwa jina la Bobi Wine.

Katika chapisho kwenye X Jumapili jioni, Kainerugaba alisema babake aliyeitawala Uganda tangu 1986, ndiye mtu pekee anayemlinda kiongozi wa upinzani Bobi Wine dhidi yake.

"Kama Mzee asingekuweko, ningemkata kichwa leo," ameandika Kainerugaba.

Bobi Wine, ambaye jina lake ni Robert Kyagulanyi, alimaliza wa pili nyuma ya Museveni katika uchaguzi wa urais wa 2021, alijibu kupitia X kwamba hapuuzi vitisho hivyo, na kusema kumekuwa na majaribio kadhaa ya kuuawa siku za nyuma.

Kainerugaba alijibu: "Hatimaye! Nimekuamsha? Kabla sijakukata kichwa, uturudishie pesa tulizokukopesha," akidai kuwa hapo awali serikali ilikuwa imemnunua Wine ili kudhoofisha upinzani.

Kainerugaba mara kwa mara hutoa machapisho yenye utata kwenye mitandao ya kijamii, ikiwa ni pamoja na tishio la 2022 la kutaka kuivamia nchi jirani ya Kenya.

Mtoto huyo wa kiume wa rais Yoweri Museveni, alisema hivi karibuni kwamba, hakuna raia atakayeongoza Uganda na kwamba hilo ni jukumu la wanajeshi au polisi.

Muhoozi Kainerugaba ambaye wengi wanaamini anaandaliwa kwa ajili ya  kumrithi baba yake, amewahi kutangaza kupitia ukurasa wa mtandao wa X kwamba hatosimama kuwania urais wa Uganda katika uchaguzi ujao.