Watu zaidi ya 100 wanyongwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121110-watu_zaidi_ya_100_wanyongwa_katika_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo
Wizara ya Sheria ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, watu 102 wamenyongwa na wengine 70 wamehukumiwa adhabu hiyo.
(last modified 2025-01-06T23:12:46+00:00 )
Jan 06, 2025 23:12 UTC
  • Watu zaidi ya 100 wanyongwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Wizara ya Sheria ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, watu 102 wamenyongwa na wengine 70 wamehukumiwa adhabu hiyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Sheria ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni kuwa watu hao, wanaume wenye umri wa baina ya miaka 18 na 35, walikuwa majambazi wenye silaha, wanaofahamika kama Kuluna, na walinyongwa kwenye gereza la Angenga kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Watu 45 tano walinyongwa mwishoni mwa mwezi Disemba na wengine 57 wamenyongwa ndani ya masaa 48 yaliyopita.

Baadhi ya duru zimeripoti kuwasili kwa ndege iliyobeba watu wengine 70 kwenye mji wa Angenga, ingawa serikali haijasema chochote kuhusu wafungwa hao.

Wizara ya sheria imesema kundi la tatu la wafungwa hao watanyongwa kama makundi mawili ya mwanzo. Hukumu ya kifo ilikuwa imefutwa tangu mwaka 1981, lakini ikarejeshwa tena mwaka 2006.

Wakati huo huo, wiki iliyopita, mahakama ya kijeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilitoa hukumu ya kifo kwa wanajeshi 13 kwa makosa ya mauaji, uporaji, na woga katika hatua ambayo inalenga kuboresha nidhamu ya jeshi. Hukumu hizi zilitolewa Jumanne iliyopita katika mji wa Lubero, Kivu Kaskazini, ambako vikosi vya Congo vimekuwa vikikabiliana na uasi hasa ule  wa kundi la M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.