Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Kenya aanika ufisadi katika maeneobunge
-
Nancy Gathungu
Ripoti ya ukaguzi imeonyesha kwamba, huenda mamilioni ya pesa za basari zilizolenga kuwasaidia wanafunzi kutoka familia masikini, zinaishia katika mifuko ya maafisa na wabunge wafisadi katika maeneobunge mbalimbali nchini Kenya.
Ripoti hiyo ya kusikitisha imetolewa wakati wanafunzi wanaripoti shuleni kwa muhula wa kwanza 2025.
Ripoti ya hivi karibuni zaidi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, iliyotolewa Desemba 2024, imefichua ubadhirifu wa fedha za Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneobunge (NGCDF), na hivyo kuwaacha wanafunzi kutoka familia maskini wakihangaika.
Ripoti hiyo inaonyesha jinsi fedha zilizokusudiwa kuwakinga wanafunzi hao zinavyoibwa katika maeneobunge mbalimbali, na basari kutolewa kwa wanafunzi hewa.
Aidha, hakuna maelezo ya majina ya taasisi za elimu, maelezo ya benki, kiasi cha basari, majina kamili ya wanafunzi na namba zao za usajili au barua au risiti kutoka kwa taasisi zinazosajili wanafunzi zilizowasilishwa kwa ukaguzi, ili kuthibitisha kuwa basari hizo zilipokelewa na taasisi za elimu.
Maeneobunge yaliyoathiriwa na sakata hilo ni pamoja na; Sabatia, Rongo, Nakuru Mashariki, Narok Magharibi na Embakasi Kaskazini. Mengine ni Webuye East, Turbo, Suba North, Sotik, Nyaribari Chache, Naivasha, Mwingi Central, Mogotio, Olkalou, Nyakach, Malindi na Westlands.