UN: Sudan kwa sasa ni sehemu pekee duniani ambako njaa imethibitishwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121122-un_sudan_kwa_sasa_ni_sehemu_pekee_duniani_ambako_njaa_imethibitishwa
Umoja wa Mataifa jana Jumatatu ulitangaza kuwepo mgogoro "wa kutisha" wa binadamu nchini Sudan, ukisema kuwa ndiyo nchi pekee ambako njaa imethibitishwa.
(last modified 2025-01-07T04:06:25+00:00 )
Jan 07, 2025 04:06 UTC
  • UN: Sudan kwa sasa ni sehemu pekee duniani ambako njaa imethibitishwa

Umoja wa Mataifa jana Jumatatu ulitangaza kuwepo mgogoro "wa kutisha" wa binadamu nchini Sudan, ukisema kuwa ndiyo nchi pekee ambako njaa imethibitishwa.

"Sudan inasalia katika mgogoro wa binadamu wa kiwango cha kushangaza," amesema Edem Wosornu, mkurugenzi wa Kitengo cha Operesheni na Himaya katika Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), akihutubia kikao cha Baraza la Usalama, na kuongeza kuwa kuna "habari za kutisha" kuhusu njaa inayoenea nchi nzima ya Sudan.

Wosornu ameashiria athari kubwa za vita vya kutumia silaha kwa raia na pia wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, na kusema: "Hali hii inaendelea kusababisha maafa kandokando na ndani El Fasher katika Jimbo la Darfur Kaskazini."

Sudan

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: "Kufika kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa, ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyoathiriwa na njaa, kunaendelea kuwa changamoto kuu."

Amesema "hali ya njaa sasa iko katika maeneo matano, ikiwa ni pamoja na kambi za IDP za Zamzam, Al Salam na Abu Shouk, na katika Milima ya Nuba ya magharibi." 

Sudan imeathiriwa na mapigano kati ya Jeshi la Taifa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) tangu Aprili 2023.