Umoja wa Mataifa: Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121128-umoja_wa_mataifa_zaidi_ya_watu_milioni_30_wanahitaji_msaada_sudan
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu zaidi ya Milioni 30 nchini Sudan, nusu yao wakiwa ni watoto wana uhitaji wa dharura wa misaada ya kibinadamu.
(last modified 2025-01-07T08:23:52+00:00 )
Jan 07, 2025 08:23 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada Sudan

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu zaidi ya Milioni 30 nchini Sudan, nusu yao wakiwa ni watoto wana uhitaji wa dharura wa misaada ya kibinadamu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, Wasudan hao wamekumbwa na hali hiyo baada ya maisha yao kutatizwa kutokana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Umoja wa Mataifa unaeleza kuwa, ili kuwasaidia watu hao, dola bilioni 4.2 zinahitaji kutoka kwa wahisani, ili kuwafikia raia wa nchi hiyo zaidi ya Milioni 30.

Sehemu nyingine ya ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema, kati ya watu hao, Milioni 20.9 wapo katika hali mbaya sana na wanahitaji msaada wa haraka kama chakula, maji safi, makaazi na dawa huku dunia ikionywa kuwa imeisahau Sudan na macho yote kuangazia Ukraine na vita vya Mashariki ya Kati.

Wito huu unakuja, baada ya hali ya ukame kutangazwa katika majimbo matano ya Sudan na hivyo kusababisha watu wengine zaidi ya Milioni 8 kuwa katika hatari ya kukabiliwa na njaa kali.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.