Wanajeshi 6 wa Nigeria wauawa katika hujuma ya Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121144-wanajeshi_6_wa_nigeria_wauawa_katika_hujuma_ya_boko_haram
Wanajeshi wasiopungua sita wameuawa nchini Nigeria  huku magari ya chuo cha kijeshi yakichomwa moto wakati kundi la kigaidi la Boko Haram liliposhambulia jeshi la Nigeria.
(last modified 2025-01-07T23:06:39+00:00 )
Jan 07, 2025 23:06 UTC
  • Wanajeshi 6 wa Nigeria wauawa katika hujuma ya Boko Haram

Wanajeshi wasiopungua sita wameuawa nchini Nigeria  huku magari ya chuo cha kijeshi yakichomwa moto wakati kundi la kigaidi la Boko Haram liliposhambulia jeshi la Nigeria.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari Jumanne, shambulio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki katika eneo la serikali ya mitaa ya Damboa, kaskazini mashariki mwa jimbo la Borno.

Shahidi mmoja alielezea shambulio hilo kama "lililopangwa vizuri" na akaongeza kuwa lilionekana kama "shambulio la kulipiza kisasi."

Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za usalama katika maeneo tofauti. Wakati nchi hiyo inapambana na uasi wa Boko Haram kaskazini mashariki, utekaji nyara na uhalifu wa majambazi ni mkubwa kaskazini magharibi.

Nigeria imekuwa ikipitia miaka 14 ya mashambulizi ya kigaidi ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 100,000 na kuwahamisha watu milioni 3, kulingana na Shirika la Kitaifa la Usimamizi wa Dharura wa nchi hiyo.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.