Serikali ya Sudan: Zaidi ya visa 500 vya ubakaji vimefanywa na wanamgambo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121156-serikali_ya_sudan_zaidi_ya_visa_500_vya_ubakaji_vimefanywa_na_wanamgambo
Zaidi ya wanawake 500 wamebakwa na wanamgambo wa Sudan tangu kuanza kwa vita dhidi ya jeshi mnamo mwezi Aprili 2023. Hayo yameelezwa na afisa wa serikali ya Sudan.
(last modified 2025-01-08T03:44:12+00:00 )
Jan 08, 2025 03:44 UTC
  • Serikali ya Sudan: Zaidi ya visa 500 vya ubakaji vimefanywa na wanamgambo

Zaidi ya wanawake 500 wamebakwa na wanamgambo wa Sudan tangu kuanza kwa vita dhidi ya jeshi mnamo mwezi Aprili 2023. Hayo yameelezwa na afisa wa serikali ya Sudan.

Sulaima Is'haq al-Khalifa, Mkuu wa Kitengo cha Serikali cha kupambana na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto amesema kuwa, mamlaka imerekodi kesi 554 za ubakaji zilizofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Msaada wa Haraka (RSF) kati ya mwezi Aprili 2023 na Desemba 2024.

Ameongeza, hata hivyo kwamba takwimu hizi zinawakilisha sehemu tu - karibu "asilimia mbili", kulingana na yeye - ya idadi ya kweli ya mashambulizi.

Baadhi ya maeneo yametengwa kabisa, mawasiliano yametatizika na wanawake wengi huepuka kuripoti unyanyasaji wa kijinsia kwa kuhofia unyanyapaa wa kijamii," amesema.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, watu zaidi ya Milioni 30 nchini Sudan, nusu yao wakiwa ni watoto wana uhitaji wa dharura wa misaada ya kibinadamu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaeleza kuwa, Wasudan hao wamekumbwa na hali hiyo baada ya maisha yao kutatizwa kutokana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka 2023 kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.