Zaidi ya watu 100,000 wakimbia makaazi yao DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121160-zaidi_ya_watu_100_000_wakimbia_makaazi_yao_drc
Idadi ya wakimbizi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inazidi kuongezeka sambamba na kuendelea ukosefu wa usalama katika maeneo ya nchi hiyo.
(last modified 2025-01-08T03:45:25+00:00 )
Jan 08, 2025 03:45 UTC
  • Zaidi ya watu 100,000 wakimbia makaazi yao DRC

Idadi ya wakimbizi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inazidi kuongezeka sambamba na kuendelea ukosefu wa usalama katika maeneo ya nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mapigano katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamepelekea zaidi ya watu 100,000 kuwa wakimbizi ndani ya wiki moja tu iliyopita.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, baina ya tarehe 1 na 3 Januari, mapigano makali kati ya jeshi na waasi wa M23 katika mji Masisi Kati, jimbo la Kivu Kaskazini, yamewahamisha makwao watu 102,000.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeeleza kuwa, "zaidi ya watu 600,000 wameyakimbia makazi yao tangu mwishoni mwa Novemba mwaka jana, na wimbi hilo la wakimbizi linaweza kuzidisha hali mbaya ya Masisi."

Wakati huo huo, vikosi vya kundi la waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, vimeuteka mji wa Masisi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Masisi unakuwa mji wa pili kutekwa na kundi hilo katika muda wa siku mbili tu kwenye jimbo la Kivu Kaskazini.

Tangu mwaka 2021, waasi wa M23 wamedhibiti sehemu kubwa ya maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuwafanya mamia kwa maelfu ya watu walazimike kuyahama makazi yao kufuatia harakati na mashambulizi ya kundi hilo.

Masisi, ambao ni mji wenye wakazi wapatao 40,000, uko takribani kilomita 80 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini Goma, ambao M23 iliuteka na kuukalia kwa muda mfupi mwaka 2012.