Kamanda wa al-Shabaab na magaidi 10 waangamizwa Somalia
Jeshi la Somalia limetangaza kuwa limefanikiwa kuangamiza magaidi 10 wa al-Shabab, kusini mwa nchi hiyo. Vilevile limetangaza habari ya kuangamizwa kamanda wa ngazi za juu wa genge hilo kigaidi atwaye Mohamed Mire katika operesheni nyingine tofauti iliyofanyika kwenye jimbo la Jubaland.
Taarifa hiyo imesema kuwa, magaidi kumi wa al Shabab wameangamizwa katika operesheni iliyofanywa kwenye kijiji cha Beer Xaani, kilichoko umbali wa kilomita 35 kaskazini magharibi mwa mji wa Kismayo wa jimbo la Jubaland, kusini mwa Somalia.
Taarifa ya awali iliyotolewa Jumatatu ilisema kuwa, kamanda wa ngazi za juu wa genge la al-Shabaabm Mohamed Mire, anayejulikana pia kwa jina la kupanga la Abu Abdirahman na ambaye alihusika na mauaji mengi ya watu wasio na hatia na ambaye alikuwa kiongozi wa kiutawala wa al-Shabaab nchini Somalia kwa miaka 15 iliyopita, naye ameangamizwa. Taarifa hiyo imethibitishwa leo na jeshi la Somalia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, magaidi hao wameuawa kwenye shambulio la anga lililofanyika katika eneo la umbali wa kilomita 10 kusini magharibi mwa Quyno Barrow na kumuua Mohamed Mire, kamanda wa ngazi za juu wa al Shabab. Tangu mwaka 2022 Mire alikuwa anasakwa kimataifa kutokana na vitendo vyake vya kigaidi ndani na nje ya Somalia.
Ripoti ya Kimataifa zinaonesha kuwa, magenge ya kigaidi likiwemo la al-Shabab yanaendelea kuwa tishio kubwa la usalama wa kimataifa. Kumekuwa kukitolewa miito ya mara kwa mara ya kuisaidia serikali ya Somalia kupambana na janga hilo la ugaidi kwa usalama wa kikanda na kimataifa.