Watu 19 wauawa Chad katika shambulio dhidi ya Ikulu ya Rais
Watu wenye silaha wameshambulia Ikulu ya Rais nchini Chad katika mji mkuu N’Djamena, na kuzua mapigano ambayo yameua washambuliaji 18 na afisa mmoja wa usalama na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Waandishi wa habari wa walisikia milio ya risasi karibu na Ikulu mjini N’Djamena, huku vifaru vikionekana barabarani, vyanzo vya usalama vimeripoti kuwa watu wenye silaha walijaribu kuvamia ikulu.
Serikali baadaye ilisema watu 19 waliuawa katika mapigano hayo, 18 kati yao walikuwa washambuliaji wa kundi la watu 24 ambalo lilifanya shambulizi hilo katika kile kinachoonekana kama jaribio la mapinduzi.
“Kuna watu 18 waliofariki na sita kujeruhiwa” miongoni mwa washambuliaji” tulipata kifo kimoja na watatu waliojeruhiwa na mmoja kati yao alijeruhiwa vibaya”, msemaji wa serikali na waziri wa mambo ya nje Abderaman Koulamallah aliziambia duru za habari.
Saa chache baada ya shambulizi hilo, Koulamallah alionekana kwenye video kwenye mtandao wa Facebook, akiwa amezungukwa na wanajeshi, akisema kwamba “hali imedhibitiwa kabisa, jaribio la kuvuruga usalama limezimwa.”
Vyanzo kadhaa vya usalama vilisema kwamba kundi la washambuliaji wenye silaha walifyatua risasi ndani ya ofisi ya rais Jumatano jioni, saa moja na dakika 45 majira ya huko, kabla ya kuzidiwa nguvu na walinzi wa rais.
Serikali ya Chad imesisitiza kuwa hali ya usalama katika mji mkuu N’Djamena iko shwari baada ya kuripotiwa ufyatuaji risasi karibu na ikulu ya rais.