Walibya wakasirishwa na hatua za kutaka kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel
Kufichuliwa maelezo ya kina zaidi ya kikao cha Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni ya Libya na mwenzake wa utawala wa Kizayuni wa Israel kumeibua wimbi la maandamano nchini Libya.
Tripoli, mji mkuu wa Libya, umeshuhudia maandamano makubwa baada ya matamshi ya waziri wa zamani wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Najla Al-Mangoush, kuhusiana na kuhusika Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa katika suala la kufanyika mkutano kati yake na Eli Kohen Waziri wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Kizayuni mwaka 2023.
Baada ya kufichuliwa taarifa kwamba, Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa alihusika na suala hilo wananchi wa Libya wamekasirishwa mno na kitendo hicho cha kutaka kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala dhalimu wa Israel.
Aidha wananchi wenye hasira wa Libya wamechoma moto bendera ya Israel na kulaani kitendo chochote cha kuwa karibu na utawala wa kibaguzi wa Israel.
Waandamanaji hao wameitaka serikali ya Libya kujiuzulu na kusisitiza kwamba, sheria ya nchi hiyo inalitambua kuwa kosa na uhalifu suala la kuwa na uhusiano na Wazayuni.
Najla al Mangoush aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya, mwaka 2023 alilazimika kukimbilia Uturuki baada ya Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya kumsimamisha kazi kwa kosa la kuonana na waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni nchini Italia.