Kinara wa upinzani nchini Msumbiji arejea kutoka uhamishoni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121240-kinara_wa_upinzani_nchini_msumbiji_arejea_kutoka_uhamishoni
Kinara wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane jana alirejea nchini kutoka uhamishoni wakati vikosi vya usalama vikifyatua mabomu ya kutoa machozi kutawanya mamia ya wafuasi wake.
(last modified 2025-01-09T23:08:48+00:00 )
Jan 09, 2025 23:08 UTC
  • Kinara wa upinzani nchini Msumbiji arejea kutoka uhamishoni

Kinara wa upinzani nchini Msumbiji Venancio Mondlane jana alirejea nchini kutoka uhamishoni wakati vikosi vya usalama vikifyatua mabomu ya kutoa machozi kutawanya mamia ya wafuasi wake.

Mondlane aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais, alionekana akishuka kutoka kwenye ndege katika uwanja wa ndege wa Mavalane, ulioko kwenye mji mkuu, Maputo.

Kiongozi huyo wa upinzani aliondoka nchini humo mwezi Oktoba mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu uliokumbwa na utata na kusababisha maandamano makubwa ya vurugu yalioitumbukiza nchi hiyo katika mzozo.

Amesema aliondoka nchini humo kwa kuhofia usalama wa maisha yake baada ya wanachama wawili waandamizi wa chama chake cha upinzani kuuawa na watu wasiojulikana mara tu baada ya uchaguzi.

Maandamano makubwa ya upinzani yaliyogubikwa na machafuko yalizuka nchini Msumbiji baada ya uamuzi wenye utata uliotolewa na mahakama kuthibitisha ushindi wa mgombea wa chama tawala cha Frelimo, ambacho kimekuweko madarakani tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa mkoloni wa Kireno mwaka 1975.

Aidha, zaidi ya wafungwa 1,500 walitoroka gereza lenye ulinzi mkali baada ya kuangusha ukuta wake wakati machafuko ya kisiasa yalipokuwa yakiendelea kufuatia uchaguzi wa Oktoba ambao matokeo yake yameibua utata. Makabiliano yaliyotokea wakati wa kutoroka wafungwa hao yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 30 mbali na wengine wengi waliojeruhiwa. Wafungwa wapatao 150 walikamatwa tena baadaye.