Wapakistan wanane wapandishwa kizimbani Tanzania kwa kosa la kusafirisha madawa ya kulevya
Raia wanane wa Pakistan wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam Tanzania wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha madawa ya kulevya.
Wapakistan hao walikamatwa na madawa ya kuulevya yenye uzito wa kilo 447.3.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana, Januari 9, 2025 na kusomewa mashtaka yao.
Washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda kosa Novemba 25, 2024 katika eneo la Navy lililopo Kigamboni, Wilaya ya Kigamboni, ambapo kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za madawa ya kulevya aina ya methamphetamine.
Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya aina heroin, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024 eneo la Navy Kigamboni, ambapo washtakiwa hao walikutwa na heroin zenye uzito wa kilo 22.53.
Washtakiwa hao ni Mohamed Hanif (50), Masdhaal Yusuph (46), Imtiyaz Ahmed (45), Tayab Pehliwam (50), maarufu kama Tayeb, Immambakhshhi Kudhabakhshi (55).
Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).
Hata hivyo kabla ya kusomewa mashtaka hayo, mmoja wa washtakiwa hao alidai kuwa, hawajui lugha yoyote zaidi ya lugha yao na kwamba, Kiingereza hawakijui vizuuri, hivyo wanaomba watafutiwe mkalimani.
Kesi zao zimeahirishwa hadi Januari 22, 2025.