Polisi: Magaidi wameua watu 21 kaskazini magharibi mwa Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121306-polisi_magaidi_wameua_watu_21_kaskazini_magharibi_mwa_nigeria
Jeshi la Polisi la Nigeria limesema katika taarifa yake ya karibuni kabisa kwamba takriban watu 21 wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2025-01-11T09:46:22+00:00 )
Jan 11, 2025 09:46 UTC
  • Polisi: Magaidi wameua watu 21 kaskazini magharibi mwa Nigeria

Jeshi la Polisi la Nigeria limesema katika taarifa yake ya karibuni kabisa kwamba takriban watu 21 wameuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Msemaji wa polisi wa eneo hilo, Abubakar Aliyu amesema katika taarifa ya karibuni kabisa kuwa, shambulio hilo lilitokea Januari 7 na lilifanywa na genge moja la kigaidi katika kijiji cha Baure cha mkoa wa Katsina wa kaskazini magharibi mwa Nigeria. 

Taarifa za huko nyuma zilisema kuwa, watu 30 waliuawa katika shambulio hilo, lakini katika taarifa rasmi ya jeshi la polisi, Aliyu amesema kuwa watu waliouawa walikuwa 21. 

Shambulio hilo lililenga Kikosi cha Walinzi wa Jumuiya ya Jimbo la Katsina (KSCWC). Walinzi hao walikuwa wakirejea kutoka katika kutoa mkono rambirambi kwa familia ya mwenzao mmoja aliyeuawa wiki moja kabla yake.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Nigeria, nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ilirekodi mauaji ya watu 614,937 kati ya Mei 2023 na Aprili 2024.

Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, ujambazi uliofanyika kitaasisi huko kaskazini magharibi mwa Nigeria ulisababisha mauaji ya watu 206,030 kwenye kipindi hicho.

Taarifa hiyo ya polisi imesema pia kwamba, maafisa wawili wa jeshi hilo wameuliwa baada ya magaidi wa Boko Haram kushambulia kituo cha polisi cha Ngazai cha mkoa wa Borno wa kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Boko Haram walifyatua risasi kadhaa na kurusha mabomu ndani ya kituo hicho cha polisi na kuua askari wawili.