Jeshi lateka mji muhimu katikati mwa Sudan
Jeshi la Sudan (SAF) jana Jumamosi liliuteka tena mji wa Wad Madani, makao makuu ya Jimbo la Gezira la katikati mwa Sudan, kutoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
Taarifa iliyotolewa jana na jeshi la Sudan imesema: "Komandi ya SAF inawapongeza wananchi wapendwa wa Sudan kwa kuingia kwa vikosi vyetu ndani ya mji wa Wad Madani Jumamosi hii asubuhi, ambapo kwa sasa wanajeshi wetu wanajishughulisha na kusafisha mabaki ya waasi ndani ya mji huo."
Nayo Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imethibitisha habari ya kutekwa tena mji wa Wad Madani na kuutaja kuwa ni ushindi muhimu kwa serikali ya Jenerali Abdel Fattah el Burhan.
Taarifa ya wizara hiyo imesema: "Ushindi huu unaashiria kukanzia kufikia mwisho jinamizi ambalo limewaelemea wananchi wa Sudan kwa takriban miaka miwili sasa kutokana na mashambulizi ya wanamgambo wa waasi."
Wakati huo huo, Jeshi la Sudan limesambaza kanda za video kutoka ndani ya makao makuu ya Komandi ya Kitengo cha 1 cha SAF huko Wad Madani, iliyokuwa ikidhibitiwa na RSF huku baadhi ya watu wakisambaza video zinazoonyesha watu wakishereheka ndani ya mji wa Wad Madani, wakiimba na kuwapungia mkono wanajeshi wa serikali ya Jenerali al Burhan.
Miji mikubwa ya Sudan, ikiwa ni pamoja na Atbara, Bandari ya Sudan, Omdurman na Kosti nayo ilishuhudia makundi ya watu yakisherehekea kutekwa tena mji wa Wad Madani na jeshi la SAF.
Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, Jeshi la Sudan SAF lilianzisha operesheni kubwa ya ardhini ili kurejesha udhibiti wa Wad Madani ambao uko umbali wa takriban kilomita 189 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Mwezi Disemba 2023, RSF ilichukua udhibiti wa Jimbo la Gezira baada ya ya jeshi la SAF kukimbia katika mji wa Wad Madani.
Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya wa vita vya uchu wa madaraka bainaya makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimtaifa yanasema kuwa, watu 29,683 wameshauawa tangu wakati huo na milioni 15 wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.