Jeshi la Kongo latwaa maeneo muhimu kutoka kwa waasi wa M23
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121388-jeshi_la_kongo_latwaa_maeneo_muhimu_kutoka_kwa_waasi_wa_m23
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa limefanikiwa pakubwa kijeshi dhidi ya kundi la waasi la M23 licha ya kushuhudiwa ongezeko la ghasia katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2025-01-13T08:09:17+00:00 )
Jan 13, 2025 08:09 UTC
  • Jeshi la Kongo latwaa maeneo muhimu kutoka kwa waasi wa M23

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetangaza kuwa limefanikiwa pakubwa kijeshi dhidi ya kundi la waasi la M23 licha ya kushuhudiwa ongezeko la ghasia katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jeshi la Kongo limetangaza kuwa limefanikiwa pakubwa kuwarudisha nyuma wanamgambo wa kundi la M23 kutoka jimbo la Kivu Kusini na kuirejesha mikononi mwake miji muhimu kadhaa katika majimbo yote mawili ya Kivu Kaskazini na Kusini. 

Guillaume Ndjike Kaiko Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amethibitisha haya katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari. Amesisitiza kuwa jeshi la Kongo limeirejesha mikononi mwake miji kadhaa muhimu iliyokuwa ikishikiliwa na wanamgambo wa M23. 

Wanamgambo wa M23 

Itakumbukwa kuwa, mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yalipamba moto wiki kadhaa za karibuni ambapo Umoja wa Mataifa ulitangaza Ijumaa iliyopita kuwa tangu Januari 1, 2025 hadi hivi sasa, zaidi ya watu 100,000 wamekimbia makazi yao katika eneo la Masisi kutokana na kuendelea mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la Kongo.

Kundi la waasi la M23 hivi karibuni lilizidisha mashambulizi yake mashariki mwaJamhuri ya Kidemokrasia ya na kuteka miji muhimu kama Katale na Masisi na kuwalazimisha watu wengi kukimbia makazi yao. Kuna makumi ya makundi ya waasi yanayoendesha harakati zao mashariki mwa Kongo, lakini waasi wa M23 ambao Kinshasa inasema ni wa kabila la Kitutsi linaloungwa mkono na Rwanda, ndilo kundi maarufu zaidi la waasi.