Etienne Tshisekedi arejea Congo baada ya kuwa nje kwa miaka miwili
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12139-etienne_tshisekedi_arejea_congo_baada_ya_kuwa_nje_kwa_miaka_miwili
Kiongozi mkongwe wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Etienne Tshisekedi amerejea Kinshasa kutoka Ubelgiji alikokwenda kwa ajili ya matibabu miaka miwili iliyopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2016 03:12 UTC
  • Etienne Tshisekedi arejea Congo baada ya kuwa nje  kwa miaka miwili

Kiongozi mkongwe wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Etienne Tshisekedi amerejea Kinshasa kutoka Ubelgiji alikokwenda kwa ajili ya matibabu miaka miwili iliyopita.

Maelfu ya wafuasi wake walifurika katika uwanja wa ndege na vilevile kujipanga katika barabara ya kuelekea kwao Limete kumlaki kiongozi huyo mkongwe wa upinzani ambaye kurejea kwake nchini kunaweza kupiga jeki harakti za wapinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mwanasiasa huyo anatarajiwa kujiunga na viongozi wengine wa upinzani hapo Jumapili kwa ajili ya maandamano na mkutano wa kisiasa wenye lengo la kimshinikiza Rais Joseph Kabila kutohairisha uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo mwishoni mwa mwaka huu.

Etienne Tshisekedi , Kiongozi mkongwe wa upinzani DRC

Harakati za Tshisekedi kama mwanasiasa wa upinzani zilianza tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kwani ndiye mmoja wa wachache tu waliothubutu kumkosoa hata Rais wa wakati huo wa Zaire Mobutu Sese Seko wakati wa utawala wake uliokuwa umepiga marufuku vyama vya kisiasa vya upinzani.

Katika uchaguzi wa 2011 akisimama dhidi ya Rais Kabila, Tshisekedi alidai ndiye aliyekuwa mshindi halisi wa kiti cha urais na wengi wa wafuasi wake wanaamini hivyo.

Rais Joseph Kabila ambaye muda wake wa uongozi unamalizika mwaka huu

Rais Kabila anayemaliza muhula wake wa uongozi mwaka huu, amekuwa akitoa wito mara kwa mara wa kufanyika mazungumzo ya kitaifa, wito ambao umekuwa ukipingwa na wapinzani. Wapinzani wanasema kuwa, lengo la mazungumzo hayo ni njama ya serikali kutaka kuakhirisha uchaguzi wa rais wa Novemba mwaka huu na hivyo kuongeza muda wa Rais Kabila kuendelea kuweko madarakani. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, uchaguzi wa rais unapaswa kufanyika mwezi Novemba ambapo Rais Kabila hapaswi kuwania kiti hicho kwa muhula mwingine.