Wapinzani Chad wapinga matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bunge
Chama cha upinzani cha Chad National Rally of Chadian Democrats (RNDT) kimekosoa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi wa ubunge kuonyesha kuwa chama tawala cha MPS kilishinda theluthi mbili ya viti.
Chama cha Patriotic Salvation Movement (MPS) cha kiongozi wa kijeshi Mahamat Deby kilishinda viti 124 kati ya 188 vya Bunge la Kitaifa katika uchaguzi wa tarehe 29 Desemba.
Matokeo hayo yametafsiriwa kama njia ya kuimarisha nguvu ya Deby katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Albert Pahimi Padacké, ambaye chama chake cha National Rally of Chad Democrats (RNDT) kilipata viti 12 pekee, alielezea mchakato huo kama "dhihaka'' akihoji uhuru na kutaka tume hiyo kutoegemea upande wowote inapotekeleza wajibu wake.
"Tulishinda katika uchaguzi wa wabunge, zaidi ya viti 50," alisema bila kutoa uthibitisho wowote.
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa mwezi Disemba 2024, yanaonesha kuwa, chama tawala nchini Chad kimekomba thuluthi mbili ya viti katika uchaguzi wa Bunge ambao ulisusiwa na sehemu kubwa ya vyama vya upinzani.
Chama cha Deby Itno cha Patriotic Salvation Movement, kimepata viti 124 kati ya 188 katika Bunge la Taifa. Kiwango cha ushiriki wa wananchi katika uchaguzi huo kilikuwa 51.56%.
Kura hiyo, ambayo pia ilijumuisha chaguzi za manispaa na tawala wa kieneo, ilikuwa ya kwanza kwa Chad katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita.