Maelfu ya Wasudan wamekimbia mapigano huko Um Rawaba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121398-maelfu_ya_wasudan_wamekimbia_mapigano_huko_um_rawaba
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, maelfu ya watu wameukimbia mji wa Um Rawaba nchini Sudan tangu kuzuka kwa mapigano wiki iliyopita kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 13, 2025 23:41 UTC
  • Maelfu ya Wasudan wamekimbia mapigano huko Um Rawaba

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, maelfu ya watu wameukimbia mji wa Um Rawaba nchini Sudan tangu kuzuka kwa mapigano wiki iliyopita kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa RSF.

Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji (IOM) limeeleza kuwa ndani ya muda wa siku tano tu, familia kutoka kwenye kaya 1,000 hadi 3,000 zimelazimika kuuhama mji wa Um Rawaba katika jimbo la Kordofan Kaskazini linalopatikana kusini mwa Sudan.

Wiki iliyopita, mapigano yalizuka katika eneo hilo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF, wakati jeshi lilipokuwa likiendesha operesheni ya kusonga mbele katika jimbo la Al-Jazira, takriban kilomita 300 kaskazini mashariki mwa Sudan.

Wakati huo huo, jeshi la Sudan limetangaza kuwa limeudhibiti mji mwingine muhimu wa Gezira, siku moja baada ya kuuteka mji mkuu wa jimbo hilo la kati, Wad Madani, kutoka kwa wanamgambo wa RSF.

Jumamosi iliyopita, jeshi na washirika wake waliuteka tena Wad Madani, mji wa pili kwa ukubwa nchini Sudan baada ya Khartoum, kufuatia siku kadhaa za mapigano makali dhidi ya RSF.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, Jeshi la Sudan SAF lilianzisha operesheni kubwa ya ardhini ili kurejesha udhibiti wa Wad Madani ambao uko umbali wa takriban kilomita 189 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya wa vita vya uchu wa madaraka bainaya makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa yanasema kuwa, watu 29,683 wameshauawa tangu wakati huo na milioni 15 wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.