Bunge jipya lafunguliwa Msumbiji katika kivuli cha migomo na maandamano
Bunge jipya la Msumbiji liliapishwa jioni ya jana Jumatatu mjini Maputo chini ya ulinzi mkali, huku migomo na maandamano yanayoongozwa na upinzani yakiligeuza jiji hilo kuwa mji wa mapepo.
Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye anaendelea kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 9, alikuwa ameitisha mgomo huo kupinga kile alichosema ni udanganyifu katika uchaguzi.
Vyama vya upinzani vya Renamo na MDM vimesusia hafla iliyoongozwa na Rais Filipe Nyusi ya kuapisha wabunge wapya, vikitaka kuhesabiwa upya kura za uchaguzi wa Bunge.
Kati ya wajumbe 250 wa Bunge la Jamhuri, 210 walihudhuria sherehe za jana Jumatatu, wakiwemo 171 kutoka FRELIMO na 39 kutoka chama cha PODEMOS.
Rais Nyusi pia alimuapisha Bibi Margarida Talapa kuwa Spika mpya wa Bunge la Msumbiji. Katika hotuba yake Bibi Talapa amekiri kuwa anachukua wadhifa huo katika wakati mgumu kisiasa lakini ameahidi kufanya kila linalowezekana ili kukidhi matarajio ya watu wa Msumbiji.
Sherehe ya kuapishwa wabunge wapya ilifuatana na maandamano katika jiji la Mapuuto, huku polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Biashara katika baadhi ya maeneo ya Maputo ziliendelea kufungwa kutokana na hofu ya uporaji.