Benki Kuu: Mapato ya Libya mwaka 2024 yalifikia karibu dola bilioni 25
Benki Kuu ya Libya ilitangaza jana Jumatatu kwamba mapato ya jumla ya nchi hiyo kwa mwaka 2024 yalifikia dinari za Libya bilioni 123.51 (takriban dola bilioni 24.95 za Kimarekani).
Benki Kuu ya Libya imetangaza hayo katika taarifa yake rasmi na kuongeza kuwa, mwaka 2024, mauzo ya mafuta ya Libya yaliingizia nchi hiyo dinari bilioni 76.7 na ziada ya dinari bilioni 13.1 kutokana na mrahaba wa mafuta.
Taarifa hiyo aidha imesema: "Mapato ya mwaka jana pia yalijumuisha dinari bilioni 22.5 kutokana na ada ya mauzo ya fedha za kigeni, wakati faida ya Benki Kuu ilifikia dinari bilioni 7."
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Benki Kuu ya Libya imesema kuwa, matumizi jumla ya nchi hiyo kwa mwaka 2024 yalifikia dinari bilioni 123.2, ambapo zaidi ya dinari bilioni 67 zilitumika kulipa mishahara, dinari bilioni 22 zilitumika katika miradi ya maendeleo, wakati dinari bilioni 16.1 zilitumika kwa bidhaa za ruzuku.
Uchumi wa Libya unategemea zaidi mapato ya mafuta. Sekta ya mafuta nchini humo imekumbwa na mgogoro wa miaka mingi ya mapigano ya silaha baina ya makundi hasimu na kufungwa mara kwa mara maeneo ya kuzalishia mafuta na bandari kutokana na mapigano hayo ya kijeshi na maandamano.
Libya haijawahi kuwa na utulivu wa kuaminika tangu mwaka 2011 wakati wa kampeni ya kumng'oa madarakani kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi. Nchi za Magharibi kupitia jeshi lao la NATO zilifanya uharibifu mkubwa wa miundombinu kwa kisingizio cha kuwasaidia wananchi wa Libya kumpindua Gaddafi, na baada ya hapo madola ya Magharibi yaliitelekeza nchi hiyo na kuicha bila ya kuwa na jeshi wala serikali yenye nguvu huku silaha nzito zikiwa zimeenea mikononi mwa makundi hasimu.