WHO: Ugonjwa unaoshukiwa kuwa Marburg waua watu wanane Tanzania
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, mlipuko unaoshukiwa kuwa ni wa ugonjwa hatari wa Marburg nchini Tanzania umewaua watu wanane, na kuonya kwamba hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini humo ni “kubwa”.
Taasisi hiyo ya afya ya Umoja wa Mataifa imesema katika taarifa yake kwamba, ilitoa taarifa kwa nchi wanachama siku ya Jumatatu kuhusu “mlipuko unaoshukiwa wa ugonjwa wa virusi vya Marburg katika mkoa wa Tanzania wa Kagera”.
“Tunayo taarifa ya kesi tisa kufikia sasa, ikiwa ni pamoja na watu wanane ambao wamefariki dunia. Tunatarajia kesi zaidi katika siku zijazo kadiri uchunguzi wa ugonjwa unavyoendelea,” Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema kwenye mtandao wa X.
Ameongeza kuwa “WHO imetoa msaada wake kamili kwa serikali ya Tanzania na kwa jamii zilizoathirika.”
Tangazo hilo linajiri chini ya zaidi ya mwezi mmoja baada ya WHO kutangaza kuwa mlipuko wa Marburg katika nchi jirani ya Rwanda ambao uliua watu 15 umedhibitiwa kabisa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt nchini Ujerumani na Belgrade huko Serbia.
Ugonjwa wa Marburg husababishwa na virusi vinavyoshabihiana na Ebola na hata dalili zake hazina tofauti kubwa na ugonjwa wa Ebola. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.