Msumbiji yamwapisha rais mpya, ghasia za baada ya uchaguzi zaua watu 300
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121490-msumbiji_yamwapisha_rais_mpya_ghasia_za_baada_ya_uchaguzi_zaua_watu_300
Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo jana Jumatano aliapishwa kuwa rais wa tano wa Msumbiji baada ya miezi kadhaa ya maandamano mabaya ambayo yamechukua roho za watu karibu 300 na kuwakosesha makazi mamia ya wengine.
(last modified 2025-01-16T04:02:12+00:00 )
Jan 16, 2025 04:02 UTC
  • Msumbiji yamwapisha rais mpya, ghasia za baada ya uchaguzi zaua watu 300

Daniel Chapo wa chama tawala cha Frelimo jana Jumatano aliapishwa kuwa rais wa tano wa Msumbiji baada ya miezi kadhaa ya maandamano mabaya ambayo yamechukua roho za watu karibu 300 na kuwakosesha makazi mamia ya wengine.

Mitaa katika mji mkuu Maputo ilionekana mitupu na maduka yalifungwa kwa hofu ya maandamano na ghasia huku Chapo akianza muhula wake wa miaka mitano kama rais wa tano wa Msumbiji.

Maandamano yameikumba nchi hiyo ya Kusini-mashariki mwa Afrika tangu Oktoba 21, 2024 wakati tume ya uchaguzi ya nchi hiyo ilipomtangaza Chapo kuwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 9. Matokeo hayo yalipingwa vikali na kambi ya upinzani na kuyaita ni wizi uliochupa mipaka.

Lucia Ribeiro, mkuu wa Baraza la Katiba la Msumbiji ndiye aliyemuapisha Chapo ambaye ni mkuu wa zamani wa mkoa wa Inhambane. Bunge jipya la Msumbiji, lenye wabunge 250 lilizinduliwa Jumatatu wiki hii.

Chapo ambaye zamani alikuwa ni mtangazaji, kiutaalamu ni mwanasheria. Ana umri wa 48 na hajawahi kushika wadhifa wowote kwenye Baraza la Mawaziri kabla ya ushindi wake wa urais.

Vyama vikuu vya upinzani vya Mozambique National Resistance Movement na Mozambique Democratic Movement vyote vimesusia sherehe za kuapishwa Chapo.

Rais huyo mpya wa Msumbiji alitangazwa mshindi wa asilimia 65 ya kura zote zilizopigwa, akifuatiwa na mpinzani wake mkuu Venancio Mondlane ambaye alipata asilimia 20 tu ya kura.

Kwa mujibu wa kundi la ufuatiliaji wa uchaguzi la Plataforma Decide, maandamano nchini Msumbiji yaliyozuka baada ya uchaguzi yameshapelekea takriban watu 300 kuuawa na maelfu ya wengine kukimbia makazi yao.