Jeshi la Sudan linachunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121518-jeshi_la_sudan_linachunguza_madai_ya_ukiukaji_wa_haki_za_binadamu
Mkuu wa jeshi la Sudan ameunda kamati ya kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati jeshi lake lililpoukomboa mji wa Wad Madani kutoka kwa wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF).
(last modified 2025-01-16T23:42:13+00:00 )
Jan 16, 2025 23:42 UTC
  • Jeshi la Sudan linachunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu

Mkuu wa jeshi la Sudan ameunda kamati ya kuchunguza madai ya ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati jeshi lake lililpoukomboa mji wa Wad Madani kutoka kwa wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF).

Sudan Kusini pia imelalamikia madai ya dhuluma dhidi zilizofanywa dhidi ya raia wake wakati wa operesheni hiyo.

Kamati hiyo itachunguza matukio ya kambi ya Taiba katika jimbo la Gezira na kuwasilisha ripoti yake ndani ya wiki moja.

RSF inadai kuwa wanajeshi wa serikali na washirika wao walilenga raia, wakiwashtumu kwa kushirikiana na wanamgambo.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Clementine Nkweta-Salami, ameelezea wasiwasi wake kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na uharibifu wa mali ambao umesababisha watu wengi zaidi kukimbia makazi yao.

Mji wa Wad Madani ulio na miundombinu ya barabara zinazounganisha majimbo kadhaa, ulikuwa chini ya udhibiti wa RSF wakati wa mzozo wa miezi ishirini.

Pande zote mbili zinakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na kushambulia kwa makombora maeneo ya makazi.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari, Jeshi la Sudan SAF lilianzisha operesheni kubwa ya ardhini ili kurejesha udhibiti wa Wad Madani ambao uko umbali wa takriban kilomita 189 kutoka mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Sudan imekuwa katika mgogoro mbaya wa vita vya uchu wa madaraka bainaya makundi mawili ya SAF na RSF tangu katikati ya Aprili 2023. Makadirio ya karibuni kabisa ya mashirika ya kimataifa yanasema kuwa, watu 29,683 wameshauawa tangu wakati huo na milioni 15 wengine wamekuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan.