HRW: Serikali za Pembe ya Afrika zimeshindwa kulinda haki za raia
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limezituhumu serikali za nchi za Pembe ya Afrika kwa kushindwa kulinda haki za raia wao.
Human Rights Watch imesema hayo kupitia taarifa yake ya kila mwaka na kueleza kwamba, mataifa mengi ya Pembe na Afrika yameshindwa kuwakinga raia wao dhidi ya migogoro ya kivita ambayo imekuwa ikishuhudiwa kati ya wanajeshi wa serikali na makundi ya waasi.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Human Rights Watch imezituhumu serikali za nchi za Afrika kwa kuwakandamiza wanaharakati na wakosoaji wa serikali.
Mkurugezi mkuu wa Human Rights Watch, Tirana Hassan, amesema kwamba serikali nyingi za nchi za Afrika zimeshindwa kuvumilia ukosoaji wa wapinzani wao na hivyo baadhi kama Kenya, zimekuwa zikiwakamata na hata kuwaua wakosoaji wa serikali.
Nchini Sudan kwa mujibu wa mkurugezi wa Human Rights Watch kanda ya Afrika, Mausi Segun, jeshi na wapiganaji wa RSF wamekuwa wakiwalenga raia kwa risasi na kuharibu miundombinu kwa makusudi.
Mausi ameongeza kuwa zaidi ya watu Milioni 12 wamekimbia makazi yao nchini Sudan kutokana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi na wapiganaji wa RSF.
Ripoti hiyo pia imeongeza kuwa pande hasimu nchini Ethiopia na Somalia, zilizuia misaada kuwafikia waathiriwa wa vita, huku maafisa wa kutoa huduma za misaada pia wakishambuliwa na hata kuuawa.
Nchini Eritrea, Human Rights Watch imeituhumu serikali kwa kuwalazimisha raia wake kujisajili kufanya kazi kwa muda mrefu, mbali na kuwasaka wakosoaji wake wanaoishi nje ya nchi na kuwakamata.