Tanzania: Sampuli zilizopimwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marbug
Serikali ya Tanzania imesema kuwa sampuli zilizochukuliwa hazijathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg, hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya.
"Mpaka tarehe 15 Januari 2025, majibu ya uchunguzi wa kimaabara…hayajathibitisha uwepo wa virusi vya Marburg".
Hayo yanajiri katika hhali ambayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa, mlipuko unaoshukiwa kuwa ni wa ugonjwa hatari wa Marburg nchini Tanzania umewaua watu wanane, na kuonya kwamba hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo nchini humo ni “kubwa”.
Wizara hiyo ilithibitisha kupokea tetesi za uwepo wa ugonjwa huo na kusema kuwa imechukua hatua za haraka.
"Tumetuma timu ya wataalamu; kufanya uchunguzi wa suala hili; kuchukua sampuli na kufanya vipimo vya maabara", taarifa ya Waziri wa Afya Jenista Mhagama imesema.
Wizara hiyo imehakikishia wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa kuwa imeimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa na kwamba itaendelea kutoa taarifa.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt nchini Ujerumani na Belgrade huko Serbia.
Ugonjwa wa Marburg husababishwa na virusi vinavyoshabihiana na Ebola na hata dalili zake hazina tofauti kubwa na ugonjwa wa Ebola. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.