Wanajeshi wa Niger wawatia mbaroni magaidi na silaha
Jeshi la Niger limetangaza kuwa, limefanikiwa kuwatia mbaroni dazeni ya magaidi na kiasi kikubwa cha silaha kupitia operesheni mbalimbali zilizoendeshwa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo ya Jeshi la Niger imesema: Miongoni mwa waliokamatwa ni watu watatu wanaoshukiwa kushiriki katika hujuma ya hivi karibuni ya bomba la usafirishaji mafuta ghafi ya Niger katika eneo la Mountseka kwenye jimbo la Tahoua.
Imeongeza kuwa: Operesheni zilizofanywa katika kipindi cha baina ya Jumapili na Jumatano zimefanikisha kugunduliwa silaha za kisasa mikononi mwa magaidi hao.
Kwa sasa Niger inakabiliana na changamoto za kiusalama zinazosababishwa na magenge ya kigaidi yanayoendesha shughuli zao kutokea nchi jirani, hususan Libya.
Hali imekuwa mbaya zaidi tangu mwaka 2011, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyoongozwa na NATO ilipouangusha utawala wa Muammar Gaddafi huko Libya, na kuacha ombwe la usalama ambalo magenge ya kigaidi yanalitumia vibaya.