Afrika Kusini yapongeza makubaliano ya kusitisha mapigano Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121536-afrika_kusini_yapongeza_makubaliano_ya_kusitisha_mapigano_ghaza
Serikali ya Afrika Kusini imepongeza makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Israel na Hamas na kuyataja kuwa ni "hatua muhimu ya kwanza" kuelekea kumaliza mgogoro wa kibinadamu huko Ghaza.
(last modified 2025-01-17T03:49:00+00:00 )
Jan 17, 2025 03:49 UTC
  •  Afrika Kusini yapongeza makubaliano ya kusitisha mapigano Ghaza

Serikali ya Afrika Kusini imepongeza makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Israel na Hamas na kuyataja kuwa ni "hatua muhimu ya kwanza" kuelekea kumaliza mgogoro wa kibinadamu huko Ghaza.

Idara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini (DIRCO) imetoa tamko hilo kufuatia Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kuafikiana na Israel kusitisha mapigano Ghaza baada ya juhudi kubwa za upatanishi za nchi kama Qatar na Misri.

Afrika Kusini imetoa mwito wa kusimamishwa amani ya haki na ya kudumu ambayo itahakikisha haki za binadamu za Wapalestina na Waisraeli zinalindwa na kuimarishwa.

Taarifa hiyo imesema: "Makubaliano ya kusitisha mapigano ni hatua muhimu ya kwanza ya kumaliza mgogoro mkali wa kibinadamu unaowatesa Wapalestina milioni 2.3 katika Ukanda wa Ghaza, mgogoro ambao Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) imeutangaza rasmi kuwa ni mauaji ya kimbari yaliyofanywa na Israel."

Aidha Afrika Kusini imesisitiza katika taarifa hiyo kwamba usitishaji vita lazima uweke msingi wa amani ya haki ambayo inapaswa kujumuisha suala la kuundwa nchi huru ya Palestina iliyoshikamana, yenye uhuru na maamuzi yake yenyewe.

Wakati huo huo, idara hiyo muhimu ya serikali ya Afrika Kusini imebainisha kuwa, msaada wa haraka na mkubwa wa kibinadamu unahitajika kwa dharura kwa ajilli ya watu wa Ghaza. Vikwazo vyote vilivyowekwa na Israel vinavyozuia kufikishwa misaada ya kibinadamu lazima viondolewe mara moja na bila ya masharti, waruhusiwe raia kupata chakula muhimu, maji, malazi na huduma za afya bila vikwazo ya vikwazo vyovyote.