Malawi yazindua mpango wa miaka 5 wa kudhibiti kipindupindu
Malawi imezindua mpango wa miaka 5 wa kudhibiti kipindupindu ambao unalenga kupunguza kiwango cha matukio ya kila mwaka ya ugonjwa huo kwa asilimia 90 na kufikia kiwango cha chini kabisa cha vifo ifikapo mwaka 2030.
Zoezi hilo lililopewa jina la Mpango wa Kudhibiti Kipindupindu wa Sekta Mbalimbali wa Malawi (MMCCP) na ambao ulizinduliwa Alkhamisi, utaimarisha uratibu na utekelezaji wa kazi za sekta mbalimbali za kuzuia na kudhibiti kipindupindu nchini humo.
Waziri wa Afya wa Malawi, Khumbize Kandodo Chiponda amesema: "MMCCP ni muhimu sana kwani rekodi zinaonyesha kwamba Malawi inakumbwa na miripuko ya mara kwa mara tangu kesi za kwanza za kipindupindu ziliporipotiwa mwaka 1973."
Kuanzia mwezi Machi 2022 hadi Januari 2025, Malawi imerikodi kesi 61,639 za kipindupindu na vifo 1,786 vinavyohusiana na ugonjwa huo. Miripuko ya mara kwa mara ya kipindupindu katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika inahusishwa na upatikanaji mdogo wa maji salama, ukosefu wa vyoo vya kutosha na kwa ujumla utamaduni na desturi mbovu za usafi katika familia.
Kwa mujibu wa waziri huyo, msururu wa majanga ya kimaumbile ikiwa ni pamoja na vimbunga vya Ana, Gombe, Hidaya, Freddy na Chido nao umezidisha hatari zilizopo na kusababisha uharibifu mkubwa kwa mifumo ya afya nchini Malawi.
Wakati huo huo, Malawi imezindua kampeni ya chanjo ya kipindupindu kwenye wilaya tano ambazo ugonjwa huo umeenea zaidi. Katika maeneo hayo, idadi ya vifo vilivyotokana na kipindupindu ni 14 na kesi zilizorekodiwa ni 263 tangu mwezi Septemba 2024.