Uhuru awahimiza Gen Z kupigania haki zao Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i121600-uhuru_awahimiza_gen_z_kupigania_haki_zao_kenya
Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kuhusu maandamano ya Gen Z, akiwataka waendelee kutetea haki zao.
(last modified 2025-01-18T07:53:06+00:00 )
Jan 18, 2025 07:53 UTC
  • Uhuru Kenyatta
    Uhuru Kenyatta

Rais Mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kuhusu maandamano ya Gen Z, akiwataka waendelee kutetea haki zao.

Akizungumza huko Gatundu Kusini, Kaunti ya Kiambu, Bwana Kenyatta ametoa matamshi yanayofasiriwa kuwa ni kuunga mkono maandamano ya vijana nchini kwa kuwahimiza kujitokeza kupigania haki zao.

Rais huyo wa zamani wa Jamhuri ya Kenya, amesema vijana kwa sasa ndio wenye nguvu na kwamba, hawana budi kupambana na wanaowahujumu. Kenyatta amewahimiza vijana kuendelea na ukakamavu na ujasiri walioonyesha mwaka uliopita, 2024, kufuatia maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali ya Rais William Ruto.

“Mpiganie haki yenu bwana, sio kukaa hapo mali yenu ichukuliwe… Mmeitolea jasho, msikubali… Pambaneni mhakikishe mmepata haki yenu. Mnaskia nyinyi?” alisema Uhuru Kenyatta.

Gen Z, Kenya

Katika maandamano ya mwaka jana ambayo yalitikisa nchi, Gen Z walijitokeza katika kila kona ya nchi kupinga kupitishwa kwa Muswada wa Fedha 2024 ambao baadaye Rais William Ruto aliufutilia mbali kutokana na mashinikizo na ghadhabu za vijana. Rais Ruto pia alilazimika kuvunja baraza lake la mawaziri na kuteua baraza jipya wakiwemo washirika wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga.